Hamad Rashid aigomea CUF
2012-01-06

 KitaifaPia amesisitiza kuwa hatambui uamuzi wa Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho lililomvua uanachama juzi pamoja na wenzake watatu, na kusisitiza kuwa bado ni mwanachama wa CUF na Mbunge wa Wawi na ataendelea kukitumikia chama kama kawaida.

Pamoja na hayo, CUF jana iliendelea kutoa matokeo ya mkutano wa Baraza hilo na kusisitiza kumtimua uanachama Hamad Rashid na wenzake watatu, huku ikiwavua uongozi wanachama wanne, kutoa karipio kali kwa watatu na wawili kukosa hatia.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Hamad Rashid alieleza amesikitishwa
kwake na Baraza hilo, lililokuwa chini ya Maalim Seif na viongozi wengine akiwamo Waziri wa Katiba Zanzibar, Aboubakar Khamis Bakar, Mwakilishi Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu na viongozi wengine wa chama kudharau amri ya Mahakama.

“Uamuzi wa Baraza hili nasema wazi ni batili, kwa kuwa kwanza halitambuliki katika Katiba ya Chama, lakini pia wakati mkutano wake ukiendelea, Mahakama Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam, ilishatoa amri ya kuusi-mamisha,” alisema Hamad Rashid.

Alisema alipoitwa kwenye mkutano huo juzi, alihudhuria na kuwa mtu wa kwanza kutuhumiwa kati ya 14 na kuhojiwa huku akisomewa tuhuma 11 zinazomkabili ambapo aliomba apewe muda wa kuzijibu tuhuma hizo lakini akakataliwa.

Alizitaja baadhi ya tuhuma hizo kuwa ni uchochezi kwa kumtaka Maalim Seif aachie nafasi moja ya ukatibu mkuu ili chama kijiendeleze, kuleta mpasuko ndani ya chama kwa kutuhumu juu ya matumizi mabaya ya uongozi na fedha na kuandika kitabu chenye siri za ndani za chama kinyume na Katiba ya chama hicho.

“Waliniomba nitoke nje ili wajadiliane kuhusu mimi kupewa muda au niendelee kujitetea, nikiwa nje wakili wangu alinitumia taarifa kwa njia ya barua pepe, kuwa Mahakama imetoa amri ya kuzuia mkutano wa Baraza hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa,” alisema.

Kesi hiyo ni ya madai namba mosi ya mwaka huu. Kesi hiyo inapinga kuanzishwa kwa Kamati ya Taifa ya Nidhamu na Maadili ya chama hicho na uteuzi wa wajumbe wake.

Alisema aliporejea ndani na kutakiwa kujitetea bila muda, aligoma na kukieleza kikao hicho kuhusu amri hiyo ya Mahakama na kwamba hawezi kuzungumza lolote kwa kuwa mkutano ni batili kwa mujibu wa amri hiyo na sheria za nchi.

Aliongeza kuwa wakati akifuatilia iwapo amri hiyo tayari imekifikia chama hicho, alipigiwa simu na wenzake na kutaarifiwa kuwa si mwanachama tena wa CUF.

“Nilistaajabu sana na kuogopa, nafahamu kuwa moja ya misingi yetu viongozi ni kuheshimu sheria za nchi, sasa huyu Makamu wa Rais ameshindwa kuiheshimu Mahakama angekuwa Rais
ingekuwaje?” Alihoji.

Amri hiyo ilitolewa juzi saa 3.40 asubuhi na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Augustine Shangwa kutokana na ombi lililowasilishwa kwa dharura mbele yake na mawakili Stola na Kusalika kutoka kampuni ya uwakili ya GF Law Chambers ya Dar es Salaam.

Alisema mkutano huo wa Baraza ulikuwa batili na uamuzi wote uliotolewa pia ni batili, hivyo
adhabu zote zilizotolewa za kusimamishwa uanachama, uongozi na makaripio makali zote ni batili.

“Mimi bado ni Mbunge, mwanachama wa CUF na wenzangu na anayepinga aende mahakamani,” alisema.

Alisema kwa taarifa alizonazo watu wengi hasa wanachama wameguswa na tukio la kufukuzwa
uanachama na wameanza kurejesha kadi za uanachama wa CUF huku wakimtaka aunde chama kipya.

“Watu wanarudisha kadi za CUF kwa wingi sana, Maalim Seif alisema ama Hamad akichafue chama au kimchafue, haya ni maneno mabaya sana kutoka kwa mtu ninayemheshimu…tutambue kufukuza watu wengi tena wazito kama sisi ni hatari kwa chama, walifukuzwa akina Mapalala (James) na Nyaruba chama kiliyumba kwa takribani miaka sita,” alisema.

Alikiri kufikiria kuanzisha chama kingine na kwamba pia wanachama wengi hasa baada ya
sakata la kusimamishwa, wamemtaka afanye hivyo, lakini alisisitiza kuwa anasubiri kesi ya msingi dhidi ya CUF iliyopangwa kusikilizwa Februari 15.

“Sitaki udikteta, waliponiomba tuanzishe chama nikawaambia tusubiri tuwe makini, tujipime
uwezo na nguvu yetu ili tukianzisha chama kiwe bora na si cha kuvuma na kufa…hata hivyo, baada ya kesi ya msingi sie wote tunaotuhumiwa, tutakutana na kujadili nini kinafuata,”
alisema.

Alisisitiza kuwa aliyosema kuhusu namna ya kukuza chama hicho kuanzia kukifufua Bara na
kutaka ufafanuzi wa matumizi ya fedha ni ya kweli, na ndio msingi wa matatizo ndani ya chama hicho, hali iliyosababisha aonekane anatenda dhambi kuhoji wanaotenda dhambi.

“Huwezi kumpa mtu zaidi ya Sh milioni 300 aende kwenye uchaguzi, halafu arudi na kura 2,000 lakini pia juzi tulipata Sh milioni 800, Sh milioni 350 zikaenda Igunga, hizi
nyingine Sh milioni 500 ziko wapi? Ukihoji unaambiwa mchochezi,” alisema.

Hata hivyo, Hamad Rashid alisema alishatangaza hatagombea tena ubunge jimboni humo katika uchaguzi ujao na kuambiwa na wapiga kura awatafutie mtu wa kumrithi.

Kuhusu hilo alisema alikataa akisema hataki wanasiasa ambao wanaingia madarakani na kusema waliandaliwa na mtu fulani na hivyo kutaka yeyote anayeona ana nia na sifa ya kuwania nafasi hiyo ajitokeze kwa hiari yake.

Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara, Julius Mtatiro, alisema wakati wakitoa uamuzi wa kumfukuza Hamad Rashid na wenzake, hawakuwa na amri ya Mahakama na kwamba mpaka jana waliendelea kutambua kwamba kiongozi huyo si mbunge wala mwanachama wao pamoja na adhabu walizowapa wenzake.

Waliovuliwa nafasi zao za uongozi ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Wilaya ya Ilala, Doni Waziri;
Masaga Masaga aliyekuwa Katibu wa Wilaya ya Ilala; Mohammed Albadawi Mwenyekiti wa Wilaya ya Temeke na Haji Nanjase, Mwenyekiti wa Wilaya ya Nachingwea.

Wengine waliopewa karipio kali ni Kirungi Kirungi ambaye alisisitiza kuwa halitambui karipio hilo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mkunduge, Tamim Tamim na Ayoub Kimangale.