Yanga, Azam macho Zanzibar
2012-01-06
Ni mchezo muhimu wa Kombe la Mapinduzi kwa timu hizo za Kundi B, ambazo zitakuwa zinamaliza michezo yao hatua ya makundi, huku kila moja ikiwa na umuhimu mkubwa na mchezo huo.

Azam inayoongoza kundi hilo ikiwa na pointi nne, inahitaji sare ya aina yoyote ifuzu nusu fainali, wakati Yanga italazimika kushinda kama itahitaji isonge mbele.

Mpaka sasa Yanga inashika nafasi ya tatu kwenye kundi lake ikiwa na pointi tatu, wakati Mafunzo inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi nne, hivyo kama Yanga itashinda leo itafikisha
pointi sita na kujihakikishia kufuzu nusu fainali, ambapo Azam majaliwa yake yatategemea
matokeo ya mchezo wa Mafunzo na Kikwajuni, ambayo inashika mkia ikiwa haina pointi.

Kama Azam na Yanga zitaenda sare, Azam itakuwa imefuzu, huku Yanga ikifikisha pointi nne na ili iingie nusu fainali itaombea Kikwajuni iifunge Mafunzo, kinyume cha hapo Yanga itakuwa imetolewa.

Yanga juzi ilifufua matumaini ya kufuzu nusu fainali ya mashindano hayo baada ya kuifunga
Kikwajuni mabao 2-0 yaliyofungwa na Jerry Tegete na Pius Kisambale.

Naye Clecence Kunambi anaripoti kuwa Yanga imeamua kupeleka kikosi chake chote kwenye mashindano hayo ya Kombe la Mapinduzi.

Awali Yanga iliamua kuacha baadhi ya nyota wake wengi wa kikosi cha kwanza jijini Dar es Salaam kuendelea na mazoezi chini ya kocha mkuu wa timu hiyo Kostadin Papic, lakini mchezo wa leo dhidi ya Azam ulisababisha mabingwa hao kubadili uamuzi wake na kuwapeleka Zanzibar.

Akizungumza na gazeti hili Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu alisema kikosi kamili cha timu hiyo kiko Zanzibar tayari kwa mchezo huo.

Alisema wameamua kupeleka jeshi lao lote Zanzibar kwa sababu ya unyeti wa mechi yenyewe kwani Azam ni timu nzuri iliyosheheni wachezaji wazuri na hivyo kuona kuna umuhimu kuongeza nguvu.

Sendeu alisema ukiondoa mshambuliaji Davis Mwape ambaye yuko nchini kwao Zambia, nyota wengine wote wa kikosi cha kwanza cha timu hiyo tayari wako Zanzibar.

Baadhi ya nyota wa Yanga ambao wamejiunga na wenzao Zanzibar jana ni pamoja na kiungo
Haruna Niyonzima, Athumani Idd, Nurdin Bakari, Hamisi Kiiza, Kenneth Asamoah, Yaw Berko, Shaabani Kado, Nadir Haroub na Chacha Marwa.

Yanga na Azam zimekuwa na upinzani mkali kwa siku za karibuni kwani Azam iliifunga Yanga mara mbili mwaka uliopita, ikishinda bao 1-0 kwenye mchezo wa kwanza wa ligi na kisha mabao 2-0 kwenye mchezo wa kirafiki.